Sunday, November 3, 2019

SIMULIZI YA KUSISIMUA : JINI WA DARAJA LA SALENDA

Image may contain: 1 person, outdoor
EPISODE :02
ILIPOISHIA
Suzana alituliza macho yake kwenye uso wa yule mwanamke aliyekuwa akiisogelea gari huku manukato makali yakizidi kujaa ndani ya gari. Kilichomshangaza zaidi umbile la yule mwanamke ambaye mwanzo alionekana kama mrefu tena mweupe lakini kila alivyomsogelea sura na umbile la yule mwanamke lilibadilika na kufanana naye kwa kila kitu. Suzana alishtuka na kufunga kioo haraka ili mtu yule ambaye yeye alimuona wa muujiza asiingie ndani ya gari. Yule mwanamke alisogea kwenye gari na kuligusa, ajabu baada ya kuligusa, alitoweka ghafla. Suzana akiwa anatetemeka alijaribu kuwasha gari kwa mara nyingine, ajabu ya Mungu gari liliwaka aliondoka eneo lile kwa mwendo wa kasi. Alipofika nyumbani kulikuwa kumekwisha pambazuka, alikwenda kuoga haraka ili awahi kanisani kwani muda ulikuwa umekwenda sana. Baada ya kuoga alirudi ndani, lakini alishtushwa na harufu ya manukato ambayo aliyasikia muda mfupi darajani gari lake lilipozima . Hakutaka kulifikiria sana lile kwa sababu muda ulikuwa umekwenda, alikwenda kwenye kabati kubadili nguo ili awahi kanisani. Baada ya kumaliza kubadili, alijikuta akiingiwa na uvivu na kwenda kukaa kwenye kitanda, haukupita muda usingizi mzito ulimshika na kulala bila kujielewa, aliposhtuka usingizini alishtuka kuiona familia yake yote imesimama mbele yake.

JIACHIE MWENYEWE
Alijiuliza kuna nini, alipojiangalia alijiona alikuwa amevaa nguo za kuendea kanisani. “Suzana upo sawa?” Mama yake alimuuliza huku akifuta machozi. “Mbona unaniuliza hivyo? Halafu mbona kama wote mlikuwa mnalia kuna nini mbona mnanitisha? “Suzana,” mama yake alimwita tena akiwa bado anamshangaa.. “Abee mama.” “Upo sawa?” Mama yake alimuuliza huku akimkagua mwanaye kwa kumshika kila kona ya mwili. “Nipo sawa mama, kwani vipi?” “Siamini kweli Mungu wa ajabu.” “Mama mbona sikuelewi nilitokewa na nini?” Suzana alizidi kushangaa. “Hebu nyanyuka kwanza.” Suzana alinyanyuka kitandani kuonesha yupo sawa, wote waliokuwa mule ndani walishukuru Mungu. “Kwani muda huu ni saa ngapi?” “Saa kumi na moja.” “Jamani ina maana sikwenda kanisani?” Suzana alizidi kujishangaa. “Kwani ilikuwaje?” Mdogo wake wa kike alimuuliza huku akionesha kumshangaa dada yake. “Hata najua basi, nashangaa kuwaona mpo mbele yangu mkitokwa na machozi kwani nilikuwa kwenye hali gani?” “Mmh, haielezeki.” “Mbona mnanitisha.” “Ulitaka kwenda kanisani misa ya ngapi?” “Ya kwanza, ooh, nimekumbuka nilihisi uchovu na kuja kujilaza kilichoendelea sikujua, kwani mama nini kimenitokea?” “Tumepigiwa simu na shoga yako kuwa upo katika hali isiyoeleweka, ndipo tulipozoana na wadogo zako kuja hapa. Tulipofika tumekukuta umepoteza fahamu hujitambui hata mapigo yako ya moyo yalionesha kusimama.” “Mungu wangu!” Suzana alishtuka sana. “Basi tulichanganyikiwa, lakini sikutaka kuamini kama kweli utakuwa umekufa, ndipo tulifanya maombi ambayo yamekufanya unyanyuke na kuonesha kama ulikuwa katika usingizi mzito. Hatuamini kama huna tatizo lolote.” “Ni ajabu kulala muda mrefu kiasi hicho sijawahi kutokewa na kitu kama hicho, lakini nipo sawa kama uchovu ni wa kawaida tu.” “Mmh, haya ni maajabu makubwa sana, kuna umuhimu wa kwenda kwanza hospitali kuichunguza afya yako.” Suzana hakutaka kubishana na familia yake, walimchukua na kumpeleka hospitali ya TMJ. Walipofika walimueleza daktari hali waliyomkuta nayo Alichukuliwa vipimo vyote ambayo havikuonesha ugonjwa wowote, waliruhusiwa kurudi nyumbani. Siku ile alichukuliwa kwenda kulala kwa wazazi wake, usiku kwake ulikuwa mrefu kuwaza yote aliyokutana nayo na hali iliyomtokea. Mpaka siku ya pili inaingia hali ya Suzana ilikuwa nzuri hakuonesha mabadiliko yoyote. Siku hiyo aliondokea kwa wazazi wake kwenda kazini, alipofika kazini alikuwa mtu mwenye mawazo mengi juu ya matukio yaliyomtokea toka alipokimbiwa na mpenzi wake kwenye ukumbi wa Club Bilicanas, matukio ya ajabu aliyoyaona baharini kwenye sherehe ya ajabu. Kingine hali waliyomkuta nayo wazazi wake kama mtu aliyekuwa amefariki, na kushangazwa na jinsi alivyoamka na kukutwa hana ugonjwa wowote zaidi ya uchovu wa usingizi. Alijiuliza hali ile imemtokea kwa sababu gani, akiwa katika dimbwi la mawazo shoga yake kipenzi Sharifa aliingia. “Vipi shoga mbona leo sikusomi?” “Mmh, shoga wee acha tu kuna mambo yamenitokea yananichanganya.” “Yapi? Hebu kaa chini nikueleze yaliyonisibu najuta kwenda club usiku.” “Yepi tena hayo shoga?” Suzana alimueleza yote aliyokutatana nayo usiku na hali iliyomkuta baada ya kumaliza kuoga ili aende kanisani na alipoamka na kukukuta watu wamemzunguka nakumueleza walimkuta akiwa kama amekufa. “Haa! Shoga unayosema ni kweli?” “Kweli kabisa.” “Huyo mtu unasema umemuona wapi?” “Daraja la Salenda” “Mmh!” Sharifa aliguna. “Mbona unaguna?” “Mbona tukio linafanana kama langu.” “Eeeh.” “Tukio gani?” “Unajua kuna mtu nilimueleza akasema eti ni uongo na uzushi, si unakumbuka kuna tukio moja lilitamba katika vyombo vya habari?” “Tukio gani?” “Lile la msichana kuota manyoya baada ya kumpa msaada ombaomba kwenye Daraja la Salenda?” “Ndiyo.” “Mimi nilikuwa mmoja wa watu walio kataa katakata kuwa ni uzushi, Suzana mimi ni mbishi sana kukubaliana na jambo linaloonekana ni la kusadikika.” “Mh.” “Basi wiki iliyopita katika majira ya saa kumi na mbili jioni nikiwa narudi nyumbani, si unajua foleni za Dar. Toka pale Palm Beach magari yalikuwa yakienda taratibu sana, tulipofika katika Daraja la Salenda magari yalisimama. Niliendelea kusubiri huku nikisikiliza nyimbo za Injili. “Nje ya magari kulikuwa na ombaomba wachache, sikushughulika nao, niliendelea kusikiliza muziki nikisubiri foleni isogee. Nilishtushwa baada yadirisha kugongwa kwa nje, niliponyanyua macho nilimuona ombaomba wa kike akitaka msaada kwangu. “Huruma iliniigia, nilifungua dirisha kidogo na kumpa noti ya elfu moja, halafu nilifunga dirisha na kuendelea kusikiliza muziki. Nilishtushwa tena dirisha kugongwa, nilipoangalia nilimuona yule yule ombaomba wa kike. Nilijiuliza ana shida gani ya kugonga tena, safari hii nilijikuta nimefungua kioo mpaka chini na kumuuliza: “Una shida gani tena?” Yule ombaomba aliyekuwa ameinama na uso wake kuzibwa na nywele nyingi alinyanyua uso wake na kunitazama, alionesha kama kunishangaa. Nilijiuliza mbona amenishangaa huenda kanifananisha na mimi nilikaza macho kumwangalia. Kilichonishangaza zaidi ilikuwa sura yake iliyofanana sana na yangu kama pacha. Moyo ulinilipuka ajabu, kuna kitu nilikiona kikitoka kwenye macho yake na kupiga kwenye macho yangu na ghafla alitoweka.” “Weee!” Suzana alishtuka. “Ndiyo maana nikasema tukio kama langu japo tofauti yake ni ndogo sana. Baada ya foleni kuanza kutembea, niliondoa gari na kwenda moja kwa moja nyumbani. Amini Suzana tukio lile wala sikulitilia maanani kwa vile sikulielewa na pia sikuwa muumini wa mambo ya kishirikina.” “Mh!” “Basi shoga, siku ile nyumbani nilikutana kimwili na mume wangu. Kama kawaida mzunguko wa kwanza ulikwenda vizuri, ajabu wa pili hakuwa na nguvu. Kila alivyojitahidi nguvu zake za kiume ziligoma.” “Mmh!” Suzana aliguna na kujitengeneza vizuri kwenye kiti chake. “Tokea siku ile mpaka leo mume wangu hana nguvu za kiume.
Je nini kitaendelea kwa SUZANA, SHEA ILI USIPITWE NA MKASA HUU UTAKAOKUSISIMUA SANA.
Previous Post
Next Post

0 Comments: