EPISODE: 01
Kamwe sitausahau mwaka 2015. Miongoni mwa mambo yanayonifanya nisiusahau mwaka huo kwanza ni namna nilivyotajirika kwa haraka kiasi kumshangaza mke wangu Martha pamoja na jamii iliyokuwa ikinizungua. Pili ni vile ambavyo utajiri wangu huo ulinipa mgongo na kuniachia kilio cha milele. Kilio ambacho kimenichochea kuandika mkasa huu ili iwe fundisho kwa vijana wenzangu na hata wale walionizidi umri.
*****
Jina langu naitwa Martin Sebastian. Kwa kweli hapo awali niliishi maisha ambayo yaliniletea fedheha kwa mke wangu na hata majirani zetu waliokuwa wakituzunguka. Siwezi kusema kwamba mke wangu hakuwa mvumilia laa hasha!! nitakuwa mchoyo wa fadhila juu yake. Mke alinivumilia kwa kipindi kirefu sana toka nipofukuzwa kazi katika kampuni ya Mohamed interprisses (MO) ambapo katika kampuni hiyo niliajiriwa kama meneja masoko. Mara zote nilikuwa mtu wa masokoni na pia nilikuwa katika kitengo cha usimamizi wa bidhaa zote zinazozalishwa katika kampuni ya (MO) na kusambazwa masokoni au madukani.
******
Sitasahau siku ile ambayo nilipokea barua kutoka kwa Mkurugenzi, barua ambayo ilihusu kusimamishwa kazi. Kwa kweli sikujua sababu za msingi za kusimamishwa kazi na hata nilipohitaji kuonana na mkurugenzi ofisini kwake nilizuiwa na viongozi ambao walikuwa na wazifa mkubwa kuliko mimi. Hakika iliniuma sana na kuamini kwamba hizo zote zilikuwa ni figisu na hila za walimwengu kuniachisha kazi. Hapo rasmi maisha yangu yalianza kubadilika taratibu na kufikia hatua ya kulalia uji. Miongoni mwa makosa ambayo naweza kusema niliyafanya na kujikuta najutia baada ya kuachishwa kazi yangu ni suala nzima la kutojipanga mapema au kuwa na kitenga uchumi kingine cha kuniingizia pesa tofauti na ajira yangu. Kosa hilo lilibadilisha maisha yangu kwa haraka sana na kuwa fukara nisiyefaa kutazamika hususani kwa watu wanaonizunguka na waliokuwa wakiyafahamu maisha yangu.
******
Sasa miezi kadhaa ilikwishayeyuka kama barafu juani toka nilipoachishwa kazi, lakini kwa kipindi hicho chote nilijitahidi kutafuta kazi lakini sikufanikiwa kupata. Hapo ndipo nikaamini ule msemo wa wahenga usemao "Kazi nzuri ni ya mwenzako" na "Mwenye kazi si sawa na yule ambaye hana kazi". Hata kama ni kazi ya kusafisha vyoo vya manispaa ni kazi.
Baada ya kutafuta kazi na kukosa kabisa, niliamua kuwa mpiga debe wa stand angalau nipate pesa ya chakula kwani kwa kipindi hicho ndicho kipindi ambacho mke wangu Martha alikuwa na ujauzito unaokaribia kujifungua. Nilijitahidi sana mke wangu asikose chochote kitu cha kuweka mdomoni lakini wakati mwingine ilimbidi alale njaa kwani niliparangana sana lakini nilirudi nyumbani mtupu. Kuna wakati niliambulia vibao kutoka kwa wapiga debe wenzangu ambao walikuwa na maguvu, walitumia maguvu yao kudhulumu wengine ili mradi tu pesa iwe yao.
Jioni moja nikiwa na mke wangu alinipa wazo.
"Mume wangu kwanini usimuendee huyu mzee jirani yetu ukamuombe msaada, hata kama sio pesa bali akusaidie upate kazi humo ndani kwake" Alinishauri mke wangu.
"Hilo ni wazo nzuri mke wangu, lakini nitaanzia wapi na toka nimefika hapa mbagala sijawahi kumuona mtu yeyote yule akiingia getini kwa huyu mzee. Muda wote geti lake limefungwa. Hata namna huko ndani kulivyo sijui" Nilimueleza mke wangu.
"Hapana mume wangu usikate tamaa mapema hivyo, siku zote mtu mwenye kupenda kujaribu ndiye hufanikiwa. Jaribu tu mume wangu pengine inaweza kuwa bahati kwako" .
*****
Maneno ya mke wangu alininyanyua kwenye kiti na kuanza kupiga hatua kuelekea nyumbani kwa mzee Mustapher. Ni mzee ambaye alikuwa na utajiri mkubwa mno na kupindukia. Alikuwa na majumba ya kifahari kila kona ya jiji la dar es salamu isitoshe alimiliki daladala zake binafsi. Kwa utajiri wake alionao niliamini kwamba kama kweli yeye ni mtu wa watu asingekosa kazi ya kunipatia.
Nilifika getini kwa mzee Mustapher, nikagusa geti kama mtu anaejaribu kulisikuma kwenda ndani. Nikashangaa kuona geti limefunguka . Sikuchelewa nikatumbukia ndani na kulirudishia geti. Kabla sijapiga hatua kuelekea ndani, gafla akatokea mlinzi.
"We...we ..wee umeingiaje humu ndani, nani kakupa ruhusa ya kupita pale getini?" Aliniuliza mlizi kwa sauti ya ukali huku uso wake ukiwa umekunjamana kama ngozi ya sokwe.
"Samahani broo, haikuwa dhamira yangu kuingia bila kukaribishwa, lakini kwasababu nimeona geti lipo wazi nikaona hakuna haja ya kugonga. Nisamehe bro".
"Hivi akili zako zipo sawa kweli. Unaingiaje kwenye nyumba ya mtu kienyeji kama vile unaingia chooni eeh?" Mlinzi alizidi kupaza sauti, wala hakuonesha kunielewa hata chembe. Mara gafla kelele zake zikamtoa mzee Mustapher ndani. Alikuwa katika mavazi ambayo kiufupi sikuyaelewa, alivalia joho kama yale wanayovaa mapadri ila lakwake lilikuwa la rangi nyeusi. Alinitizama usoni kama simba aliyeona kitoweo kisha akaachia cheko kubwa tena la ajabu. Kicheko kile kilipokoma, nikashangaa kuona wanaume sita wakitokea mule ndani alipotokea mzee Mustapher. Nao walikuwa wamevalia majoho ya rangi tofautitofauti, wengine walivalia meusi kama lile la mzee Mustapher na wengine walivalia mekundu.
Ningali bado katika hali ya mshangao ama bumbuwazi. Gafla mzee Mustapher akatoa amri nikamatwe kisha niingizwe ndani.
"Mkamateni huyo haraka, mumlete ndani". Aliamuru mzee Mustapher kisha akageuka kuelekea ndani. Punde si punde nilinyakuliwa na wale wanaume sita. wakanibeba juu juu kama mbuzi mwenye mguu mbovu ambaye hawezi kabisa kutembea kuelekea machinjoni. Hamadi waliponifikisha ndani wakanitua chini. Gaflai nilitaka kuachia uyowe kwa kile nilichokiona mbele yangu lakini mmoja kati ya wale watu sita aliniwahi na kuniwekea viganja vyake vya mkono mdomoni..
Je nini kiliendelea? SHARE KWA MARAFIKI ZAKO ILI UWEZE KUSOMA MKASA HUU KWA MTIRIRIKO MZURI.
0 Comments: