Monday, October 28, 2019

SOMA KISHA JIFUNZE

Image may contain: 1 person, smiling, outdoor
MTUNZI : Lovi Pius Kijogoo

Leo mikono yangu imegeuka sanda ya mwanangu!, mikono yangu imegeuka jeneza la mwanangu!, mikono yangu imegeuka chumba cha kuhifadhia maiti ya mwanangu!, mikono yangu Leo imegeuka kaburi la mwanangu.

Hakika maumivu ya moyo yanaua haraka kuliko Hata sumu, naumia sana kwanini mwanangu umeamua kufariki ukiwa katika mikono yangu jamani ni pigo kubwa sana katika nafsi yangu,

"uchungu wa mtoto u katika nyonga ya mama yake" tazama ni uchungu kiasi gani ninaoupata kuona mwanangu ukiwa umepoteza uhai wako.

Mwanangu siamini kama mikono yangu imegeuka kuwa kitanda cha milele kwako, tazama mwili wako ulivyobeba hisia mbali mbali za ugumu wa maisha tuliokuwa nao,

Nisamehe sana mwanangu najua njaa imechangia kuchukua uhai wako, Mwanangu ulichoka kuvumilia mateso ya hapa Duniani ivyo ukaamua uoneshe Upendo wa dhati kwa mama yako ukamzawadia kifo cha utulivu katika mikono yake.

Mwanangu siamini kama nimekubeba katika mikono yangu ukiwa umefariki tayari, maumivu na machungu uliyokuwa nayo najua ni siri ya moyo wako,

Najua fika umekuwa ukinionea sana huruma mama yako ndio maana ukaamua ufariki ukiwa katika mikono yangu.

Mwanangu acha niendelee kukubeba katika mikono yangu Labda unaweza ukaamka nakuja kunifuta machozi yanayonichuruzika,

Kama Dunia ndivyo ilivyo basi ijaribu kuwa na huruma kwa waja wake, Mwanangu mbavu zake zinahesabika, afya yake imedhoofika mpaka nafsi na ndio maana moyo wake ukasema hauko tayari kuyavumilia magumu hayo na ndio maana ukaamua upumzike.

Mwanangu nasema asante! umeamua mikono yangu iwe ndio jeneza lako, Kila napokutazama mwanangu jinsi ulivyolegea yaani pumzi hauvuti tena Bali mwili wako umepoa na kuwa wa baridi sana,

Jamani mwanangu nilitamani uzungumze nami kabla ya kufa kwako najua fika umeondoka ukiwa na Chuki sana kwa viongozi wetu waliotutelekeza sisi wakazi wa vijijini.

Mwanangu nasema asante nami nimekubali mikono yangu iwe kaburi lako, nimekumbuka siku niliyokuzaa kwani ilikuwa chini ya mti Mkubwa ambao ulikuwa umeharibiwa sana kwa risasi,

Na kipindi nashikwa na uchungu ilisikika milio ya risasi pembeni ya mti huo jamani vita sio nzuri viongozi wetu tuoneeni huruma sisi wananchi wenu.

Nasema tena asante sana mwanangu kwa kuamua mikono yangu iwe jeneza lako, njaa Pamoja na ukame vimesababisha mwanangu kufariki, nani wa kunifuta machozi? Nani wa kurudisha tumaini langu tena.

Mwanangu nilitamani sana ungekuwa Mkubwa ili uzunguke ulimwenguni kote na kuelezea madhara ya vita pamoja na njaa.

Jamani mwanangu siamini kama nazungumza na mwanangu aliyefariki tayari, jamani vita! vita! vita imeniachia maumivu ya milele nilipoteza mume wangu aliyekatwa katwa ovyo kwa mapanga kisha nikashuudia wazazi wangu wakichomwa moto mpaka kufa!, Duh.! Siamini kama sina ndugu tena katika ulimwengu huu ama kweli vita umeamua kuuponda moyo wangu.

Narudia tena katika sauti ya unyonge na huzuni ya aina yake nasema asante Mwanangu uliyeamua mikono yangu kawako iwe sanda, jeneza, chumba cha kuhifadhia maiti na kaburi pia.

Asante sana mwanangu upumzike kwa amani. Nakusihi sana Mwanangu wasamehe viongozi wote waliopelekea sisi kuyaishi maisha Haya ya kinyonge na kimasikini. Kila mtu anaowajibu wa kupaza sauti kupinga vita Pamoja na tatizo la ukame linalokaribisha njaa, Nasema Mwenyezi Mungu awabariki Nyoooote.
USISAHAU KUSHARE APP YETU PENDWA NA WENGINE
Previous Post
Next Post

0 Comments: